JINSI YA KUPANDA UFUTA KWA WELEDI SANA
KILIMO BORA CHA UFUTA
Ufuta (sesamum
indicum)ni zao linalolimwa kwa wingi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma,
Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga na ukanda wa chini katika mikoa ya Rukwa na
Mbeya. Zao hili hulimwa kwa ajili ya chakula na biashara. Mbegu za zao hili
huwa na wastani wa mafuta kiasi cha asilimia 45.

MAMBO YA KUZINGATIA WA KATI WA KUZALISHA MBEGU •
Chagua aina ya mbegu inayotoa mazao mengi na bora, inayovumilia
mashambulizi ya magonjwa na wadudu, inayokomaa mapema na kutoa mafuta mengi.
• Chagua mbegu inayokomaa kwa pamoja ili kurahisisha uvunaji na pia
kuepuka upotevu wa zao shambani. • Aina nyeupe ya mbegu ya ufuta hupendelewa
zaidi kuliko aina nyeusi.
UPANDAJI
Panda mbegu nusu inchi chini ya udongo, inchi sita umbali wa mbegu na mbegu na
futi mbili nafasi ya msitari na msitari, kabla ya kupanda hakikisha ardhi
imelowana vya kutosha na upande mbegu masaa mawili au matatu baadae
MBOLEA
Ufuta unahitaji rutuba ya kutosha ili kutoa mazao bora. Katika kudumisha rutuba
ya udongo, tumia kilimo cha mzunguko wa mazao au weka mbolea za asili pale
inapobidi.
PALIZI
Dhibiti magugu kwa kupalilia ili kuruhusu ufuta kutumia vizuri unyevu na
virutubishi. Magugu mengine huwa ni maficho ya wadudu waharibifu wa zao la
ufuta.
MAGONJWA NA WADUDU
Ufuta hushambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali ambao huweza kusababisha
upungufu na ubora wa mazao. Hivyo kagua shamba mara kwa mara hasa kwenye maua
na mapodo ili kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili zamashambulizi,
chukua tahadhari mapema kabla ya uharibifu mkubwa haujatokea.
MAANDALIZI KABLA YA KUVUNAKAGUA SHAMBA
• Kagua shamba kuona kama ufuta umekomaa. • Ufuta hukomaa, kati ya miezi mitatu
na minne tangu kupanda kutegemea aina.
• Aina ya ufuta usiokuwa na matawi hukomaa mapema kuliko ile yenye
matawi.
• Ni muhimu kuwahi kuvuna ili kuepuka ufuta kupukutikia shambani.
DALILI ZA KUKOMAA UFUTA SHAMBANI
• Kwa kawaida majani hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya manjano na
hatimaye kudondoka.
• Mashina hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya kahawia.
VIFAA VYA KUVUNIA
• Kamba
• Siko
• Panga
VIFAA VYA KUKAUSHIA
• Sehemu ya kukaushia yenye Sakafu ya saruji
• Maturubai
• Sakafu safi
USAFIRI
• Mikokoteni
• Matela ya matrekta
• Magari
KUVUNA
• Vuna ufuta mapema kabla mapodo kukomaa sana na kuanza kupasuka na kuachia
punje.Mapodo ya ufuta yaliyokomaa sana yakiguswa au kutikiswa na upepo hupasuka
na kuachia mbegu, hali inayosababisha upotevu mkubwa.
• Mbegu za ufuta ni ndogo na zikidondoka chini ni vigumu kuziokota.
Vilevile mbegu zilizodondoka ni vigumu kuzitenganisha na uchafu.
• Uvunaji wa ufuta huhusisha ukataji wa mimea yenye mapodo kwa kutumia vyombo
vya mkono kama panga kwa kukata mashina.
• Kwa aina za ufuta zenye mapodo yanayopasuka, uvunaji ufanyike wakati mimea
bado ni kijani ili kuepuka upotevu wa mbegu.
• Aidha uvunaji ufanyike wakati hakuna upepo wala jua kali.
• Baada ya kukata mashina yafunge katika mizigo midogo na kuweka katika
vyombo vya kusafirisha kama vile mikokoteni, matela au magari hadi sehemu ya
kukaushia.
• Panga mizigo midogo kwa kusimamisha katika malundo madogo yasiyozidi mizigo
minane kwenye sehemu safi za kukaushia.
KUKAUSHA
Mapodo ya ufuta hukaushwa yakiwa yamefungwa katika vitita. Vitita huwekwa kwa
kuegeshwa kwenye fremu ya kukaushia kwa muda wa wiki mbili hadi tatu kutegemea
hali ya hewa. Fremu hii huwekwa juu ya turubai au sakafu ili kuzuia upotevu wa
punje kutokana na kupasuka kwa mapodo.
KUPURA
Upuraji hufanyika kwenye turubai, mkeka au kwenye sakafu safi.
• Vitita hupigwa taratibu kwa kutumia mti au hutikiswa vikiwa vimegeuzwa
vichwa chini ili kuruhusu punje za ufuta kudondoka kwenye sakafu safi au
turubai.
KUPEPETA NA KUPEMBUA
Kupepeta na kupembua hufanywa ili kuondoa takataka kama vile mawe, vipande vya
mapodo,vijiti na vumbi.Njia bora ya kupepeta na kupembua ni kwa kutumia mikono.
• Ufuta huwekwa kwenye vyombo kama vile ungo kwa kiasi cha kilo mbili hadi
tatu. Ufuta hurushwa hewani kwa kasi ndogo na takataka nyepesi huchukuliwa na upepo.
Zile nzito huondolewa kwa mikono.
KUFUNGASHA
Mbegu za ufuta zilizo safi huwekwa kwenye vifungashio kama vile magunia madogo
ya aina ya juti ya ujazo wa kilo 50.
• Fungasha mbegu za ufuta kwenye magunia yenye uzito usiozidi kilo 50.
Kabla ya kufungasha hakikisha mbegu zimekauka hadi kufikia unyevu wa asilimia
10.
KUHIFADHI
• Panga magunia ya ufuta juu ya chaga.
• Panga kwa kupishanisha ili kuruhusu mzunguko wa hewa kati ya magunia.
KUSINDIKA MBEGU ZA UFUTA
Ufuta husindikwa kupata bidhaa ya mafuta ambayo hutumika katika mapishi
mbalimbali. Mafuta hukamuliwa kwa kutumia njia za asili na kwa kutumia mashine.
Njia za asili zina ufanisi mdogo ukilinganisha na zile za kukamua kwa mashine,
hivyo ni vyema kutumia mashine. Kuna mashine za aina mbili zinazotumika kukamua
mafuta; mashine za mkono na zile zinazoendeshwa kwa injini au mota ya umeme.
Mashine za mikono zinazotumika zaidi hapa nchini ni za aina ya daraja (Bridge
press) na Ram.
KUKAMUA KWA MASHINE YA DARAJA
Mashine ya daraja ni moja ya mashine za kisasa zinazoweza kukamua mafuta ya
ufuta. Mashine hizi huendeshwa kwa mikono na zina uwezo wa kukamua mafuta kwa
asilimia 68 hadi 72. Inaweza kukamua kilo 25 za ufuta kwa saa moja. Ili kupata
ufanisi mzuri wa mashine hii, ni muhimu ufuta uwe na unyevu wa kati ya asilimia
11 na 13. Iwapo unyevu utakuwa chini ya kiwango hicho inashauriwa kunyunyizi
maji kwenye ufuta kabla ya kukamua.
VIFAA VYA KUKAMULIA MAFUTA
• Mashine ya daraja
• Sufuria • Vifungashio
• Mifuko midogo ya nguo au viroba vyenye upana wa sentimita 20 na urefu
wa sentimita 20.
• Chombo cha kukinga mafuta.
• Chujio safi
• Lebo
• Lakiri Malighafi
• Mbegu za ufuta safi
• Maji safi
UKAMUAJI MAFUTA
• Nyunyuzia maji kidogo kwenye ufuta ili kuongeza unyevu kufikia asilimia 11
hadi 13. Mafuta hutoka vizuri kwenye kiwango hicho cha unyevu.
• Jaza ufuta kwenye vifuko vya nguo au viroba
• Vipange vifuko hivyo kwenye silinda na kuanza kuzungusha mhimili hadi mafuta
yaanze kutoka kupitia matundu ya silinda.
• Acha kwa muda mafuta yaendelee kutoka kisha endelea kuzungusha mhimili hadi
mafuta yaishe. Mhimili ukiacha kuzunguka ni dalili kuwa mafuta yamekwisha.
• Weka lebo na lakiri
• Hifadhi mahali pakavu na pasipo na mwanga mkali.
UKAMUAJI
• Anika mbegu za ufuta juani kwa kuzitandaza kwenye mabati ili zipate joto la
kutosha.
• Lengo la kuanika mbegu juani ni kurahisisha ukamuaji wa mafuta.
• Jaza mbegu za ufuta kwenye mpare wa kulishia
• Funga wenzozuia (HANDLE)ili mbegu za ufuta zisitoke.
• Nyanyua wenzozuia mpaka juu ili kuruhusu mbegu za ufuta kuingia kwenye
silinda.
• Shusha wenzozuia chini ili kuruhusu pistoni kusukuma mbegu za ufuta ziingie
ndani ya eneo la shindilio
. • Nyanyua tena wenzozuia mpaka juu na kushusha na wakati huohuo ukiendelea
kujaza mbegu za ufuta kwenye mpare wa kulishia. Wenzoinua ukiwa mzito ni dalili
kuwa msukumo wa kutosha umejengeka. Msukumo huo utasababisha mafuta kutoka.
• Mafuta yanapoanza kutoka legeza wenzozuia ili kuruhusu mashudu kutoka.
• Chuja na hifadhi mafuta kwenye vyombo safi vyenye mifuniko
vilivyochemshwa.
MATUMIZI
Mafuta ya ufuta
hutumika katika mapishi mbalimbali ili kuongeza ladha. Pia husaidia kuleta
nguvu na joto mwilini. Mbegu za ufuta huchanganywa na vyakula mbali mbali kama
mikate, keki, mboga na kadhalika.
Ni mkoa gani ambao huzalisha zao la ufuta kwa wingi admin
ReplyDeleteMkoa wa singida
Delete